Vigogo Chadema Kyela Wavuliwa Uongozi kwa Usaliti


Mwenyekiti wa Chadema Wilaya ya Mbeya Mjini, Saadati Mwambungu pamoja na wajumbe 19 wa kamati ya utendaji wa wilaya hiyo, wamevuliwa uongozi baada ya kutuhumiwa kukihujumu chama.

Hatua hiyo ilifikiwa juzi jioni na uongozi wa Chadema Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, chini ya mwenyekiti wake, Dk Stephen Kimondo na Mratibu wa Kanda, Frank Mwaisumbe na kuweka wilaya hiyo chini ya uangalizi wa uongozi wa Mkoa wa Mbeya ndani ya siku 30 wakati wakiendelea na uchunguzi.

Mratibu wa Chadema katika Kanda hiyo, Frank Mwaisumbe alisema jana kuwa baada ya kufanyia kazi tuhuma 17 zilizowasilishwa kwao na wanachama wa chama hicho wilaya, walibaini kuwa tuhuma saba kati yake zina ukweli dhidi ya viongozi hao hivyo wakafikia uamuzi wa kuwasimamisha na kuwataka kurudisha mali zote za chama hicho ndani ya siku 30.

“Ni kweli jana (juzi) tulifika Kyela na katika kikao chetu na kamati ya utendaji ya wilaya tulipowahoji ilionekana tuhuma saba zina ukweli na baadhi ya watuhumiwa walikiri. Miongoni mwa tuhuma hizo ni matumizi mabaya ya fedha na mali za chama, kutoshiriki vyema Uchaguzi Mkuu wa mwaka jana hadi tukapoteza jimbo, hususani siku ya kuhesabu kura za jumla viongozi walikimbia.

“Siku ile ya uchaguzi wa mwaka jana kuna vijana wetu walikamatwa wakituhumiwa kuvunja ofisi pale halmashauri ya Kyela na wakahukumiwa, lakini hakuna kiongozi yeyote ngazi ya wilaya aliyethubutu hata kwenda kuwaona pale gerezani hadi walipojinasua wenyewe,” alisema Mwaisumbe.

Alisema kutokana na mkutano wao wa juzi wajumbe wake kutotimia ili kufikia uamuzi halali wa kuwachukulia hatua zaidi, uongozi wa Kanda uliamua kuwasimamisha na chama kuwa chini ya mkoa, huku ukifanyika utaratibu wa kuitisha mkutano mkuu ambao utawajadili kwa kina na kuona kama watafukuzwa moja kwa moja au la.

Mwambungu alipoulizwa juu ya kutimuliwa kwao, alikiri huku akisisitiza kwamba tuhuma zilizotolewa hazina ukweli wowote kikatiba, na badala yake zimetengenezwa na ‘genge’ la watu wachache kwa uchu wa madaraka, lakini hana kinyongo kusimamishwa uongozi kwa kuwa ipo kikatiba ndani ya Chadema.

Alisema; “Kwanza ni heshima kwa kuwa jambo hili lipo kikatiba. Lakini katika mkutano wa juzi akidi ya wajumbe haikutimia kwani Chadema Wilaya ya Kyela ina wajumbe 349 wa mkutano mkuu, lakini kwa juzi wajumbe waliohudhuria walikuwa 120 tu.

“Ndiyo maana uongozi wa Kanda ulitoa siku 30 za kufanyika mkutano mkuu utakaowajumuisha wajumbe wote 349 na ndipo itakapofahamika… kama ni kufukuzwa au kuendelea na uongozi,”alisema.

Mwambungu alisema kati ya wajumbe 19 wa kamati ya utendaji ya wilaya, wajumbe saba waliamua kujiuzulu uongozi na baadaye wakaungana na wengine ambao waliunda tuhuma hizo kwa lengo na kuuangusha uongozi ikiwa ni maandalizi ya uchaguzi mwaka 2020

No comments:

Powered by Blogger.