RAIS MAGUFULI AMNG'OA KIGOGO MWINGINE IKULU
Kwa mujibu wa mabadiliko yaliyotangazwa na Ikulu jana, Rais Magufuli amemwondoa Ikulu Gelasius Byakanwa, ambaye alikuwa
msaidizi wake wa karibu.
Taarifa ya iliyotolewa jana na Kurugenzi ya Mawasiliano Ikulu, ilisema mpaka mabadiliko hayo yanafanyika jana, Byakanwa alikuwa Katibu wa Rais Msaidizi Mwandamizi.
Taarifa hiyo iliyomnukuu Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi John Kijazi ilisema Rais Magufuli amempeleka kigogo huyo kuwa Mkuu wa Wilaya Hai mkoa wa Kilimanjaro, kuchukua nafasi ya Antony Mtaka.
Katika uteuzi mpya wa wakuu wa mikoa hivi karibuni, Mataka aliteuliwa na Rais kuwa Mkuu wa Mkoa wa Simiyu.
Kigogo huyo wa Ikulu anakuwa wa pili kuondolewa Ikulu baada ya Sefue aliyeondolewa katika mabadiliko yaliyotangazwa Machi 7.
Nafasi ya Sefue ambaye alitumikia nafasi hiyo kwa miezi mitatu ya utawala wa awamu ya tano, ilichukuliwa na Kijazi aliyekuwa Balozi wa Tanzania nchini India.
Wakati wa mabadiliko hayo, Rais Magufuli aliahidi kumpangia kazi nyingine Sefue.
Uteuzi wa kigogo huyo kuwa DC pia ni dalili kwamba Rais Magufuli anakamilisha-kamilisha orodha ya wakuu wapya wa wilaya ambayo imekuwa ikisubiriwa kwa shauku kubwa.
Watu wengi wamekuwa na shauku ya kujua nani watarejeshwa kwenye safu hiyo mpya na nani ambao watatupwa huku sura mpya zikitarajiwa kuonekana kwenye utawala huo wa awamu ya tano.
Tangu aingie madarakani, Rais Magufuli amekuwa akipunguza baadhi ya watumishi Ikulu na kuwarejesha kwenye wizara mbalimbali walikokuwa awali.
Alipoingia tu Ikulu Novemba 5 mwaka jana alifuta baadhi ya vitengo vilivyokuwa Ikulu kikiwemo kile cha Lishe ya Rais na cha kukaribisha wageni binafsi.
Katika siku zake 100 za kwanza tangu alipoingia madarakani, tayari Serikali yake imewafukuza kazi vigogo zaidi ya 70 kwa tuhuma mbalimbali ikiwamo za ufisadi.
Rais Magufuli aliwang’oa vigogo wapatao 23 wa Mamkala ya Bandari (TPA) na kuvunja Bodi ya Wakurugenzi ya mamlaka hiyo kutokana na upotevu wa makontena zaidi ya 11,000.
Bodi hiyo ilikuwa na vigogo kadhaa akiwamo Naibu Spika wa Bunge, Dk. Tulia Ackson na Mkurugenzi wa zamani wa Mamlaka ya Udhibiti ya Nishati na Maji (EWURA), Haruna Masebu.
Hatua ya kuvunjwa kwa bodi hiyo, ilitokana na kushindwa kuisimamia vyema Bandari ya Dar es Salaam, hali iliyosababisha makontena 2,716 kutolewa bandarani bila kulipia kodi na kuisababishia Serikali hasara ya mabilioni ya shilingi.
JIPU LA RAHCO
Rais Magufuli pia alimsimamisha kazi Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni Hodhi ya Rasilimali za Reli (RAHCO), Mhandisi Benhadard Tito ambaye tayari amefikishwa mahakamani kwa makosa ya matumizi mabaya ya madaraka.
Uamuzi huo ulilenga kupisha uchunguzi wa kina kutokana na ukiukwaji mkubwa wa taratibu za manunuzi uliobainika katika mchakato wa utoaji wa zabuni ya ujenzi wa reli ya kati.
JIPU LA TAKUKURU
Rais Magufuli pia alitengua uteuzi wa Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Dk. Edward Hosea, Desemba 16, mwaka jana.
Akizungumzia uamuzi huo, aliyekuwa Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue, alisema ulichukuliwa baada ya Rais Magufuli kutoridhishwa na namna taasisi hiyo ilivyokuwa ikitekeleza wajibu wake katika kukabiliana na rushwa, hususani kwenye upotevu wa mapato ya Serikali katika bandari ya Dar es Salaam.
Alisema Rais Magufuli alijiridhisha kwamba utendaji kazi wa Dk. Hosea usingeendana na kasi yake, hivyo alimteua aliyekuwa Naibu Mkurugenzi Mkuu wa Takukuru, Valentino Mlowola kuwa Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa taasisi hiyo.
JIPU LA NIDA
Januari 26, mwaka huu Rais Magufuli alitangaza kumsimamisha kazi Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA), Dickson Maimu ili kupisha uchunguzi dhidi yake.
Maimu alisimamishwa pamoja na maofisa wengine wanne wa NIDA kwa tuhuma za ubadhirifu wa fedha za Serikali.
Maofisa hao ni Mkurugenzi wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano, Joseph Makani, Ofisa Ugavi Mkuu, Rahel Mapande, Mkurugenzi wa Sheria, Sabrina Nyoni na Ofisa Usafirishaji, George Ntalima.
Dk. DAU wa NSSF
Magufuli alimwondoa kwenye nafasi ya ukurugenzi aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa NSSF, Dk. Ramadhani Dau na kumteua kuwa Balozi.
MAWAZIRI
Desemba 10, mwaka jana, Rais Magufuli alitangaza baraza lake la mawaziri ambalo alianza kwa kuteua mawaziri 19, ingawa wizara ni 18. Mawaziri sita kati ya hao ni wanawake.
MAKATIBU NA MANAIBU
Katika mwendelezo wa kuhakikisha kuwa wale anaowateua wanakubaliana na kasi yake, Rais Magufuli aliwapa kiapo cha utii makatibu wakuu wa wizara na manaibu wao.
Akiwaapisha kiapo hicho aliwaeleza wazi kwamba yule atakayeshindwa kufanya kazi ni bora ajiondoe mwenyewe na kupisha wengine watumikie wananchi.
AWARUDISHA NYUMBANI MABALOZI ‘MIZIGO’
Rais Magufuli aliiagiza Wizara ya Mambo ya Nje, Afrika Mashariki na Ushirikiano wa Kikanda na Kimataifa kuwarejesha nyumbani mara moja mabalozi wawili ambao mikataba yao ilikuwa imemalizika.
Mabalozi hao, Batilda Buriani aliyekuwa Japan na Dk. James Msekela aliyekuwa Italia walitakiwa kukabidhi kazi kwa ofisa mkuu au mwandamizi aliye chini yao.
Pia alimrejesha nyumbani Balozi wa Tanzania nchini Uingereza, Peter Kallaghe na kuagiza Wizara ya Mambo ya Nje, Afrika Mashariki na Ushirikiano wa Kikanda na Kimataifa kumpangia kazi nyingine.
No comments: