MAALIM SEIF AANIKA MBINU 13 ZA KUMKABILI DK. SHEIN


Zanzibar. Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF), Maalim Seif Sharif Hamad amesema wanachama wa chama hicho watatumia maazimio 13
ya Baraza Kuu la chama hicho kuipinga Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) kwa njia ya amani na demokrasia inayoendana na misingi ya Katiba na sheria za nchi.

Amesema baada ya Baraza Kuu kutoa maazimio hayo, kinachofanyika sasa ni kupanga mikakati ya kuyatekeleza huku akiwataka Wazanzibari kuhakikisha wanayatimiza huku wakidumisha amani na utulivu.

Maalim Seif ambaye pia alitangaza kutoutambua uteuzi wa wajumbe wa Baraza la Mapinduzi uliofanywa na Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein, ametoa kauli hiyo ikiwa imepita wiki moja tangu kaimu mwenyekiti wa kamati ya uongozi wa chama hicho, Twaha Taslima kutangaza maazimio hayo ya Baraza Kuu.

“Tutaibana Serikali hii ‘haramu’ mpaka itakaposalimu amri. Katika dunia ya leo huwezi kuongozwa na watu ambao hawana ridhaa kutoka kwa wananchi,” alisema Maalim Seif jana katika mkutano wake na waandishi wa habari alipokuwa akieleza mwelekeo wa CUF baada ya kususia uchaguzi wa marudio uliofanyika Machi 20 mwaka huu.

Alisema CUF lazima iipinge Serikali iliyopo madarakani kwa sababu imepatikana kinyume na sheria.

“Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984 na marekebisho yake ya mwaka 2010 katika ibara ya 9(1), inalazimisha Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kuwa na muundo wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK). Ibara ya 39, 39A na 42 za Katiba zimeeleza namna SUK inavyoundwa,” alisema Maalim Seif huku akisisitiza kuwa hilo halijafanyika.

Huku akitaja maazimio matatu; ya kutoyatambua matokeo ya urais, uwakilishi na udiwani; kuwataka wananchi kuwakataa watawala wabovu na kuzitaka jumuiya za kimataifa kuinyima misaada Serikali ya CCM, Maalim Seif alisema utekelezaji wake utaitikisa Serikali iliyopo madarakani.

CUF ilisusia uchaguzi wa marudio baada ya Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), Jecha Salim Jecha kufuta matokeo ya urais, uwakilishi na udiwani, akisema kulikuwa na ukiukwaji wa sheria na kanuni za uchaguzi.

Akiwa na viongozi mbalimbali wa chama hicho akiwamo Naibu Katibu Mkuu – Zanzibar, Nassor Ahmed Mazrui, Maalim Seif alisema: “Hivi sasa tunapanga mikakati madhubuti ya utekelezaji wa maazimio hayo ili kuona maamuzi ya watu wa Zanzibar yanaheshimiwa.”

Alisema ana uhakika kuwa mikakati wanayoipanga itazaa hatua ambazo zitaibana Serikali iliyopo madarakani na hatimaye itasalimu amri kwa wananchi wa Zanzibar.

“Kwa mujibu wa Katiba, wananchi ndiyo wenye mamlaka ya kuiweka madarakani Serikali wanayoitaka si mtu mwingine,” alisema.

Maalim Seif alizipongeza jumuiya za kimataifa na washirika wa maendeleo kwa msimamo waliochukua wa kukataa kubariki ubakaji wa demokrasia kwa kuinyima misaada Serikali ya CCM.

“Natoa wito wachukue hatua zaidi  dhidi ya watawala hawa waovu zikiwamo kuwawekea vikwazo vya kusafiri na kufuatilia akaunti zao za fedha nje ya nchi na kuchunguza matendo yao ya uhalifu dhidi ya binadamu.

“Wananchi waliodhulumiwa haki zao wanaziunga mkono hatua hizo wakiamini kwamba CCM ni lazima iwajibishwe kwa matendo yake maovu dhidi yao.”

Alisema nchi zinazoendelea haziwezi kujiendesha bila msaada, huku akisisitiza kuwa katika bajeti ya mwaka 2015/16 fedha za maendeleo Zanzibar zilikuwa Sh300 bilioni lakini zilizotolewa ni Sh46 bilioni, “...kwa mtindo huu nani kasema utaweza kujitegemea?”

Alisema CUF watapeleka taarifa za kufutwa kwa uchaguzi wa Oktoba 25 na kutangazwa kurejewa Machi 20 katika mashirika mbalimbali, ikiwamo Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC) ili kuona ni namna gani litafanyiwa kazi na haki ipatikane.

Alisema mwaka 2009 yeye pamoja na Rais mstaafu wa Zanzibar, Aman Abeid Karume waliwaongoza Wazanzibari kuzika siasa za ubaguzi na chuki lakini hivi sasa siasa hizo zinaanza kurejeshwa na CCM jambo ambalo ni hatari kwa mustakabali wa nchi.

“Natoa wito kwa Wazanzibari wenzangu kukataa kurudishwa kwenye siasa za aina hii na kila mmoja afanye lililomo katika uwezo wake kuendeleza maelewano, umoja, upendo, mshikamano na undugu,” alisema.

Alisema CUF ilipochukua uamuzi wa kususia uchaguzi iliamua kusimama juu ya uamuzi unaoheshimu misingi ya kikatiba ambayo Wazanzibari wameamua kuwa ndiyo inayopaswa iongoze na iendeshe nchi.

“Tulijua kuwa uamuzi huu utakuwa na athari kwa CUF na Zanzibar lakini tulijua na tuliamini pia kwamba athari hiyo haiwezi kuwa kubwa zaidi kuliko gharama ya kuikanyaga Katiba na sheria za nchi yetu. Gharama za kupiga teke demokrasia, haki za binadamu na utawala wa sheria,” alisema.

No comments:

Powered by Blogger.