Fomu No. 21B yatesa ‘ubunge’ wa Wenje

Ezekia Wenje, mbunge wa zamani wa Jimbo la Nyamagana
FOMU namba 21B yenye matokeo ya vituo mbalimbali kwenye Jimbo la Nyamagana, Mwanza ndiyo inayomtesa Ezekia Wenje, mbunge wa zamani
wa Jimbo la Nyamagana, anaandika Moses Mseti.
Kutokana na vuta nikuvute ya upatikanaji wa fomu hiyo, Wenje jana amelazimika kuiomba Mahakama Kuu Kanda ya Mwanza kuifunga kesi yake ya kupinga matokeo ya ubunge yaliompa ushindi, Stanslaus Mabula (CCM).
Wenje amefikia hatua ya kuifunga kesi hiyo namba 3 ya mwaka 2015 baada ya ombi lake la mahakama kupokea fomu namba 21B yenye matokeo ya vituo mbalimbali vya jimbo hilo kutupiliwa mbali.
Akitupilia mbali ombi hilo Kakusulo Sambo, Jaji wa Mahakama Kuu, Kanda ya Sumbawanga amesema kuwa, upande wa mpeleka maombi ulishindwa kutoa sababu za msingi katika ombi lao, ni kwanini walichelewa kupeleka mahakamani fomu namba 21B.
Jaji Sambo amesema kuwa, mpeleka maombi kortini alipewa siku 10 za kupeleka fomu hiyo lakini alishindwa kufanya hivyo, kitendo ambacho kinaipa mahakama nafasi ya kutupilia mbali ombi lao.
“Katika ombi lenu hili mnaomba kupokelewa kwa fomu namba 21B, lakini hamjatoa sababu za msingi ni kwa nini mlichelewa kuleta mahakamani fomu hiyo, hivyo naliondoa ombi hili,” amesema Sambo.
Kufuatia kuondolewa kwa ombi hilo, Deya Outa, wakili wa aliyrpeleka maombi mahakamani ameiomba mahakama hiyo kuifunga kesi hiyo, kwani haitakuwa na nguvu ya kutolewa ushahidi mahakamani.
Ouata ameiambia mahakama hiyo kuwa, fomu namba 21B yenye matokeo ya kila kituo ndio ilitakiwa kutolewa ushahidi na mashahdi wake lakini baada ya kukataliwa ombi lao hakuna sababu za msingi mashahidi kutoa ushahidi.
Amesema, “fomu hii ndio ilitakiwa mashahdi kuja kutoa ushahidi wao, sasa kama ombo letu limekataliwa hawa mashahidi watatoa ushahidi gani? Hivyo tunaomba mahakama kuifunga kesi hii,” amesema Outa.
Upande wa mjibu maombi unaotetewa na wakili, Constatine Mtalemwa umeiomba mahakama kuwapa muda wa kwenda kupitia hoja hiyo iliyotolewa na upande mpeleka maombi ili kuona kuna hoja ya kujibu. Jaji Sambo ameghairisha kesi hiyo hadi kesho.

No comments:

Powered by Blogger.