CUF Wamuomba Rais Magufuli Na Waziri Mkuu Majaliwa Waingilie Kati Mgogoro Wa Umeya Tanga


Chama  cha Wananchi (CUF) kimemuomba, Rais John Magufuli na Waziri Mkuu, Kasim Majaliwa, kutumia
busara kumaliza mgogo wa umeya katika jiji la Tanga kama ilikuwa kwenye mgogoro wa umeya jiji la Dar es Salaam na kuagiza uchaguzi huo urudiwe. 


Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Naibu Katibu Mkuu wa CUF Tanzania Bara, Magdalena Sakaya, alisema chama hicho hakimtambui meya aliyeko hivi sasa kwa madi kuwa si mshindi halali katika uchaguzi uliofanyika Desemba 19, mwaka jana.

Alidai katika uchaguzi huo, mgombea wa CUF, Rashid Jumbe, ndiye aliyeshinda dhidi ya mgombea wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Seleman Mustafa, lakini ushindi wake uliporwa na msimamizi wa uchaguzi huo kwa kutangaza matokeo tofauti.

Sakaya alisema kilichotokea katika uchaguzi huo ni uporaji wa matokeo, jambo ambalo limesababisha meya huyo kutokubalika.

“Kutokana na mvurugano uliopo katika suala hilo, shughuli za maendeleo katika jijini la Tanga zimesimama na tangu kufanyika kwa uchaguzi huo hakuna kikao hata kimoja cha baraza la madiwani kilichofanyika kwa sababu madiwani wa CUF wamegoma kushiriki,”alisema.

“CUF inamuomba Rais Magufuli ama Waziri Mkuu kutumia busara kama zile zilizotumika kumaliza mgogoro wa umeya Dar es Salaam ili vikao vya baraza la madiwani viweze kuanza na kuharakisha shughuli za maendeleo ya jiji,” alisema Sakaya.

Kwa upande wake, Mbunge wa Tanga Mjini (CUF), Mussa Mbarowe, alisema ana amini Rais atatumia busara kumaliza mgogoro huo ili kuwanusuru wananchi wa jiji hilo.

No comments:

Powered by Blogger.