Maalim Seif Afunguka wakati Wazanzibar wakipiga Kura........"Kilichotokea Zanzibar ni mipango iliyopangwa na CCM"


Aliyekuwa Mgombea Urais kupitia Chama cha Wananchi (CUF), Oktoba 25
, mwaka jana, ambaye pia ni Makamu wa Kwanza wa Rais Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad, amesema hatma ya Wazanzibar iko mikononi mwa Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Maalim Seif alitoa kauli hiyo baada ya kuulizwa ni nini hatma ya Zanzibar baada ya uchaguzi wa marudio uliofanyika jana.

“Mimi sijui, waulizeni CCM wao ndiyo wametengeneza hali hii, wao ndiyo wamekusudia na wanajua wanaipeleka wapi nchi hii, watasema wao,” alisisitiza Maalim Seif.

Aliyasema hayo alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari baada ya kutembelewa na Vijana wa Baraza la Chama cha Demokrasia na Maendeleo Chadema-Bavicha jijini Dar es Salaam jana kumjulia hali.

Baada ya kufutwa kwa uchaguzi wa Oktoba 25, mwaka jana, hali ya kisiasa ya Zanzibar imedaiwa kuwa tete haswa kutokana na CUF kudai hawatambui kufutwa kwa uchaguzi huo msimamo wao wakitaka mshindi atangazwe.

Maalim Seif alisema CCM wanafahamu wazi kwamba mshindi aliyeshinda katika uchaguzi wa wa Okotoba 25, ni nani, lakini wameamua kufanya hivyo na kuifikisha Zanzibar hapo ilipo sasa.

Alisema miaka mitano iliyopita kulikuwa kumepatikana maridhiano Zanzibar na walikuwa wameanza kwenda vizuri, lakini kinachoonekana hivi sasa wameanza kuwarudisha nyuma kwa kuvuruga tena maridhiano hayo na kuanza kuleta uhasama.

“Hapo nyuma kulikuwa na uhasama wa kisiasa Zanzibar halafu ukaisha, lakini hivi sasa wanaurudisha, CCM ndiyo wameamua iwe hivyo,” alisema Maalim Seif.

Kadhalika, Maalim Seif alisema anaamini Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (Zec), Jecha Salim Jecha, ametumwa kuitafutia kura CCM.

“Jecha ametumwa kuitafutia kura CCM, lakini ijulikane kwamba hata wafanye vyovyote watakavyofanya, Wanzanzibari ndani ya mioyo yao, wanafahamu Rais wao ni mimi,” alisema Maalim Seif na kuongeza:

“Kinachotokea Zanzibar ni mipango iliyopangwa na CCM ambao pamoja na kwamba wanamfahamu mshindi ni nani katika uchaguzi wa mwaka jana, lakini wameamua kufanya hicho wanachofanya hivi sasa.”

Aidha, alisema kwa sasa hataki kusema chochote, isipokuwa anasubiri Rais atangazwe.

Maalim Seif yuko jijini Dar es Saalam kwa mapumziko mafupi baada ya kuugua na kuruhusiwa kutoka hospitali zaidi ya wiki moja iliyopita.

No comments:

Powered by Blogger.