CUF: Tunahofia mauaji Z’bar

Maalim Seif Sharrif Hamad, aliyekuwa mgombea Urais wa Zanzibar kwa tiketi ya CUF, nyuma ni wafuasi wake
CHAMA cha Wananchi (CUF) kinahofia mauaji visiwani Zanzibar endapo kitatoa kauli ya kuwataka wanachama na wananchi kusaka haki yao
kutoka mikononi mwa Serikali ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), anaandika Happyness Lidwino.    
Nassor Ahmed Mazrui, Naibu Katibu Mkuu wa CUF Zanzibar akizungumza na mtandao huu leo amesema, CUF ina hofu ya Mungu na kwamba, wanajua endapo watakapowafungua minyororo wananchi wao, Zanzibar haitakalika.
Amesema, chama hakioni hoja ya kusababisha mauaji kutokana na dhuluma inayofanywa na Dk. Ali Mohammed Shein, Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Zanzibar na viongozi wa Serikali ya Chama Cha Mapinduzi (CCM).
“Dunia ukiiendea mbio mwisho wake ni kuangamia, tunajua dhulma huwa haidumu. Inahitajika sana subra ili kuokoa maisha ya wengi. Tunajua kwamba dhulma imetendeka lakini hakuna shaka hakutakuwa na mwananchi atakayeuawa kwa sababu yetu,” amesema na kuongeza;
‘’Sisi tumetulia, hatuna shaka tunatizama tu watakachoamua kufanya sisi tutakaa kimya kwani hatuko tayari wananchi wetu wamwage damu.”
Mazrui amesema kuwa, kwa sasa wananchi wengi wanaweza kutojua kwanini CUF imekaa kimya na kwamba “kukaa kimya pia si ujinga, muda ukifika wananchi wataelewa kwa nini tuliamua kujitoa kwenye uchaguzi na kukaa kimya.’’
Magdalena Sakaya, Naibu Katibu Mkuu wa CUF Bara ameuambia mtandao huu kuwa, wananchi watulie kwakuwa chama chao hakitayumba.
Amesisitiza kwamba, CCM sio mbabe isipokuwa busara na muono wa mbali wa CUF ndio mafanikio ya uchaguzi unaofanyika leo na kwamba, chama chao hakirudi nyuma katika harakati zake mwaka 2020.
“Hakuna marefu yasiyo na nchi,” amesema Sakaya na kuongeza “ wakati wa CCM kuachia nchi unafika, hili halipingiki. Tunajua wananchi hawatuelewi lakini watatuelewa.”
Kuhusu uendeshwaji wa chama Sakaya amesema, “kwa asilimia kubwa chama kinaendeshwa na wananchi wenyewe na ruzuku inayopatikana ni ndogo sana kwa hiyo chama kitaendelea kuwa imara hata kama ruzuku itapungua.”
Kuhusu hatua zitakazochukuliwa na chama baada ya kumalizika kwa uchaguzi Sakaya amesema, hivi sasa chama kipo kimya kikisubiriwa ‘rais wao haramu’ atangazwe kisha kitajua ni hatua gani za kuchukuliwa kwa kuwa hadi sasa pia kuna baadhi ya viongozi wao wapo kizuizini.
‘’Serikali na CCM hadi sasa bado hawaamini kama wanaendesha uchaguzi wao wa mabavu salama kwa kuwa, wanachokifanya sio kizuri hakiwapendezi wananchi ndio maana walikuwa wanajihami kwa kuleta vifaa vya vita hata kuwakamata viongozi wetu wakihofia wanaweza kuvuruga uchaguzi,” amesema Sakaya.

No comments:

Powered by Blogger.