Chadema waibua jambo Umeya Dar
Mbunge wa Jimbo la Ukonga, Mwita Waitara akizungumza na waandishi wa habari
WAKATI Serikali ikitoa mwaliko wa wajumbe wanaotakiwa kupiga kura kumpata Meya wa Jiji la Dar es Salaam, Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimealika Watanzania wote kwenda kushuhudia uchaguzi huo.
Akizungumza jijini Dar es Salaam jana, Mbunge wa Jimbo la Ukonga, Mwita Waitara alisema anashangazwa na barua ya mwaliko wa uchaguzi huo ambayo imealika wajumbe pekee.
“Barua hiyo tuliyoipokea ina shida kwa sababu wanasema wajumbe peke yao ndiyo wanaoalikwa kwenda katika viwanja vya Karimjee, mkutano ule unapaswa kuwa huru kwa watu wote na waandishi wa habari,” alisema Waitara.
Waitara alisema Chadema wana hofu kuwa kuzuia wananchi kushuhudia tukio hilo, kunaonesha kuwa kuna nia ovu ambayo inataka kufanyika. Alisema wamemwandikia barua Kaimu Mkurugenzi wa Jiji kwamba wao wamealika wafuasi wao kwa kuwa sheria inaruhusu.
“Kusema kwamba kuna zuio la watu wasio wajumbe, ina maana kuna jambo wanaficha, sasa sisi tunaalika Watanzania wote waje kushuhudia tukio hilo la kupatikana Meya wa Dar,” alisema Waitara.
Katika hatua nyingine, Meya wa Ilala, Charles Kuyeko (Chadema), amemshangaa Rais John Magufuli kwa kumsifia Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, kuwa anachapa kazi na kwamba na uwezo wa kuweka watu ndani, kwa madai kuwa huko ni kumpa kichwa.
No comments: