TANESCO Yapeleka Maombi ya Kupandisha Bei Ya Umeme

SHIRIKA la Umeme (Tanesco) limepeleka maombi
kwa Mamlaka ya
Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (Ewura), kuomba kupandisha bei ya nishati
hiyo, kinyume na matakwa ya Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter
Muhongo ya kushusha bei hiyo.
Taarifa ya Ewura kwa umma iliyotolewa kwenye vyombo vya habari
jana, imeeleza kuwa maombi hayo yamepokewa Jumatano ya wiki hii na kutaka wadau
kujitokeza kujadili uhalali wa nyongeza hiyo siku mkutano huo utakapoitishwa.
“Mamlaka inaanzisha mchakato wa kupata maoni ya wadau, ili kujua
uhalali wa maombi ya nyongeza ya bei za huduma iliyoyapokea kutoka Tanesco,” imeeleza taarifa hiyo.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, Tanesco iliwasilisha ombi husika
kulingana na Sheria ya Umeme namba 131, inayoitaka Ewura kufanya mabadiliko ya
bei zinazotozwa na mtoa huduma mara moja kila baada ya miaka mitatu.
“Pendekezo la wastani wa badiliko la bei za umeme ni asilimia
1.1 kuanzia Aprili mosi 2016 na asilimia 7.9 kuanzia Januari mosi 2017,”limeeleza tangazo hilo.
Mapendekezo hayo japo ya kisheria, lakini yanapingana na msimamo
wa Waziri Muhongo, ambaye tangu alipoapishwa kushika wadhifa huo, alielezea kusudio
lake la kutaka bei ya nishati hiyo ishushwe.
Profesa Muhongo alikwenda mbali na kuagiza Tanesco, Ewura na
Shirika la Maendeleo ya Petroli (TPDC), kumpelekea mapendekezo ya kushuka kwa
bei ya umeme kuanzia mwanzoni mwa mwaka huu.
Katika maagizo hayo, Profesa Muhongo alihoji kwa nini bei ya
umeme isishuke, wakati gharama za uzalishaji wa umeme wa kutumia mafuta
zimeshuka kutokana na kupungua kwa bei ya mafuta katika soko la dunia.
Kutokana na maombi hayo ya Tanesco, Ewura imewataka wadau wa
nishati wanaopenda kutoa maoni yao kwa maandishi, kufanya hivyo kwa kutuma
maoni yao kwa Mkurugenzi Mkuu wa Ewura, ghorofa ya saba jengo la LAPF Pensions
Fund Tower, mkabala na Kijiji cha Makumbusho, Kijitonyama Dar es Salaam.
Kwa watakaotuma kwa njia ya posta, wameombwa kufanya hivyo kwa
kutumia Sanduku la Posta 72175, Dar es Salaam, Tanzania, simu namba (+255-22)
2123853-4; Fax namba (+255-22) 2123180; Barua pepe info@energyregulators.org au
tovuti http://www. energyregulators. org.
Taarifa hiyo imeeleza kuwa mamlaka hiyo pia, itaitisha mikutano
ya wazi ili kukusanya maoni kuhusu mapendekezo hayo kutoka kwa wadau
mbalimbali, wakiwamo Baraza la Wawakilishi wa Watumiaji wa Huduma (CCC); Baraza
la Ushauri la Serikali (GCC) pamoja na wananchi kwa ujumla.
No comments: