Moyo wa Chuma wa Mbwana Samatta na Kilichowashinda Boban na Henry Joseph Kucheza Mpira wa Kulipwa Ulaya
Wahenga wana usemi wao ati ‘mvumilivu hula
mbivu’ usemi
huu kwa tafsiri ya kawaida kabisa humaanisha
jinsi ambavyo binadamu anaweza kula matunda mazuri endapo tu atavumilia shida
na jua wakati wa utafutaji wa tunda hilo.
Kwa utamaduni wetu wa Kiswahili hakuna kitu
kigumu kama kuishi kwa ndugu, mbali na nyumbani kwenu. Ni rahisi
sana kutafuta vijisababu ati unateswa na shangazi yako ama shemeji ili tu urudi
ukajitanue nyumbani kwenu.
Mwaka 2013 niliposafiri kwenda Johannesburg,
Afrika Kusini kwa ajili ya mashindano ya Guinness Football Challenge
niliamini kuwa hakuna kitu kigumu kama kwa Mtanzania wa kawaida kuishi
umangani, hali ya hewa (baridi kali), chakula (hakuna chipsi mayai) na
mambo mengine mengi ya Kiswahili tuliyoyazoea, kupiga soga na marafiki na
mambo kama hayo, inahitaji kujitolea sana kuishi.
Ukisoma historia ya safari ya Yaya Toure kutoka
Abdjan hadi sasa anakula maisha Etihad, akihama kutoka nchi ya joto Cote d’Ivory
hadi Moscow sehemu yenye baridi kali, kubaguliwa rangi na matatizo ya
lugha, lakini alikomaa hadi sasa sio tu siye waafrika wenzake bali
wazungu wanamtukuza, kweli mvumilivu hula mbivu.
Haruna Moshi Boban alipata fursa ya kucheza ligi
kuu ya nchini Sweden, tukafurahi kwamba sasa Tanzania inaanza kupata
wachezaji wa kimataifa, lakini kilichomfanya Boban arudi Dar es Salaam,
bila shaka tumekielewa kidogo mara baada ya kusoma hapo juu, nchi
nyingi za wenzetu, zina mazingira magumu sana kwa mtu kupata bangi na
mambo mengine kama hayo, la! kwa gharama kubwa, ni ngumu sana kwa
uswahili wetu huu.
Unakijua alichoshauriwa ndugu yangu Mrisho
Ngassa asiende Sudan, na kuamua kubakia zake ligi ya Bongo? Je, nini
kilimshinda Henry Joseph Shindika hata arudi nyumbani akishindwa maisha ya
Norway? Inahitaji moyo wa chuma wa Yaya Toure, kufikia kilele.
Wiki hii nikiwa natazama mahojiano maalumu kati
ya watangazaji wa Sports Bar ya Clouds Tv na mshambuliaji wa Tanzania
anayekipiga Genk Ubelgiji, nilikumbwa na hisia kubwa na kumwomba Mungu wangu
azidi kumtia nguvu na kumfanyia wepesi Mbwana Samatta afikie kilele cha
matarajio yake.
Maisha ya Mbwana Samatta ni magumu mno kwa
wachezaji ama yeyote mwenye moyo wa karatasi na mtu asiye mvumilivu.
Ingawa ni mapema bado sana, lakini kwa
Mbwana Aly Samatta, ni ngumu sana kukubali yaishe huko umangani ili arudi
kuandikwa na magazeti yetu hapa ya sports, tumuombee.
Safari hii ya Mbwana Aly Samatta ni zaidi ya
funzo kwa wanamichezo wote nchini pamoja na yeyote yule mwenye kutaka kuziishi
ndoto zake. Juhudi na uvumilivu wa Samatta utampeleka sehemu ambayo
hakuna mtu yeyote amewahi kufikiria kuna siku Tanzania itakua na mwakilishi
wake, kila la kheri Mbwana Ali Samatta.
By Na Simon Chimbo

No comments: