PIngamizi la mgombea wa ubunge singida kutoka kwa msindai latupiliwa mbali

PINGAMIZI lililokuwa limewekwa na mgombea wa ubunge Jimbo la Singida Mjini kupitia Chadema dhidi ya mgombea wa CCM limetupiliwa mbali kutokana na kukosa mashiko.
Mgombea Mgana Msindai wa Chadema alimwekea pingamizi wa CCM, Mussa Sima kabla ya uamuzi kutolewa jana na Msimamizi wa Uchaguzi wa jimbo hilo.

Kaimu Msimamizi wa Uchaguzi, Jimbo la Singida mjini, Gerald Zephyrin alisema Msindai alidai fomu za Sima hazikuwa sahihi kwa mujibu wa kanuni
, taratibu na sheria za uchaguzi.
Pia Msindai alidai kuwa barua ya kumthibitisha Sima kugombea ubunge ilikuwa imesainiwa na mtu ambaye hakubaliki kisheria kwa madai kwamba, ilisainiwa na Mary Maziku, ambaye siyo Katibu halisi wa CCM mkoa wa Singida.
“Katika kujiridhisha, iwapo Maziku siyo mtu stahiki wa kumthibitisha Sima kugombea ubunge jimbo la Singida Mjini, niliwasiliana na CCM Lumumba jijini Dar es Salaam na kujibiwa kwa maandishi kuwa Maziku ndiye Katibu wa CCM mkoa wa Singida,” alisema Zephyrin.
Ilielezwa kwamba, Mary Maziku amechukua nafasi ya Mary Chatanda na kwamba barua ya kumthibitisha Sima wakati wa kura za maoni aliandika Chatanda ingawa wakati wa kumthibitisha kugombea nafasi ya ubunge, ameandika Maziku.
Wakati huo huo, aliyekuwa mgombea ubunge kwa tiketi ya UPDP, Victoria Msusu ameenguliwa kwenye kinyang’anyiro hicho baada ya kushindwa kuwasilisha fomu yake kwa wakati na kutolipa ada ya fomu hiyo Sh 50,000.
Kwa mujibu wa Kaimu msimamizi huyo wa uchaguzi, wagombea ubunge jimboni humo waliopitishwa ni Mussa Sima (CCM), Jeremia Wandili (ACT -Wazalendo), Mgana Msindai (CHADEMA) na Mwanamvua Haji (CUF).
-HABARI LEO

No comments:

Powered by Blogger.