HANS ‘ANAVYOIIBUA’ YANGA KIMATAIFA, ANASTAHILI SIFA

Kocha wa Yanga Hans van Pluijm na Niyonzima wakielekea kwenye vyumba vya kubadilishia nguo wakati wa mchezo kati ya Yanga dhidi ya Friends Rangers
Kazi kubwa ambayo imefanywa na kocha wa Yanga SC, Hans Van der Pluijm katika timu
hiyo ya ‘Mitaa ya Twiga na Jangwani’ inaweza kupimwa kwa kukumbukwa mara ya mwisho ilipocheza na Simba SC katika mchezo wa ‘Nani Mtani Jembe-2’.
Kipigo cha mabao 2-0 cha Disemba, 2014 kiliashiria mwisho wa zama za Mbrazil, Marcio Maximo ambaye alijiunga kama mkufunzi wa Yanga, Juni 2014 akichukua nafasi ya Hans aliyekuwa amemaliza mkataba wake wa muda mfupi (Miezi 6) mara baada ya kumalizika kwa msimu wa 2013/14.
Yanga ikiwa karibu kutwaa ubingwa wake wa pili mfululizo wa ligi kuu Tanzania Bara (VPL) msimu huu na ikiwa imeshinda michezo yake mitatu kati ya 6 ya klabu Afrika msimu huu, itakuwa ikipigana vita nyingine leo Jumamosi katika michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika.
Miezi 18 ya Hans, 67 na klabu hiyo, anakwenda kucheza mchezo wake wa kwanza wa ‘play off’ dhidi ya Esperanca ya Angola. Mafanikio makubwa ya Yanga katika kipindi cha miaka miwili yanaelekea kupatikana, wakati huu timu ya Hans ikiwa imefanikiwa kufika hatua ya 16 mara 3 ndani ya miaka miwili katika michuano ya CAF, ni lazima apewe sifa nyingi.
Alikuja Yanga akiwa mwalimu mwenye miaka 65. Umri ambao wakati mwingine watu husema ‘umepitwa na wakati ‘ katika soka la kisasa. Katika mchezo wa soka, ili kocha upate hamasa ya wachezaji, unahitajika kwanza kuwa na hamasa hiyo wewe mwenyewe.
Kuwa na matarajio ya kufanikisha mipango mikubwa kama kocha husaidia kwani huwaingia wachezaji pia. Baada ya kuondoa tishio la kukosa ubingwa kwa mara ya pili mfululizo, njaa ya mafanikio aliyo nayo Hans imemuwezesha kuingoza Yanga hadi hatua ya 16 bora ya michuano ya Shirikisho Afrika mwaka 2015 ambapo walitolewa na Etoile du Saleh ya Tunisia kwa jumla ya magoli 2-1.
Ilikuwa kama njia yake ya kuweka kiwango cha juu katika timu kwa ajili ya mafanikio ya siku za baadae. Hans amekuwa akifanya kazi yake kwa bidii, na mazoezi anayofundisha yamekuwa na ubora labda kuliko yote waliyowahi kupata wachezaji wa Yanga. Mara nyingi ari ikiwa hivyo katika timu huwa ni kipindi kizuri mno kwa wachezaji kukuza viwango vyao kiuchezaji.
Watazame wachezaji kama magolikipa, Ally Mustapha ‘Barthez’ na Deogratius Munish ‘Dida,’ au walinzi Juma Abdul, Oscar Joshua, Kelvin Yondan na nahodha Nadir Haroub, hawa ni wachezaji ambao wamejitahidi kupandisha viwango vyao chini ya Hans.
Kitendo cha Hans kuisaidia tena Yanga kufika hatua ya 16 katika ligi ya mabingwa msimu huu (walikotolewa na kuangukia katika kombe la Shirikisho) ni kama kimeiinua upya timu hiyo katika michuano ya CAF ambako mara ya mwisho walifanikiwa kufika kwa hatua hiyo mwaka 2007. Umakini wake katika kila jambo ni mfano wa kuigwa.
Hana wachezaji wazuri sana lakini kila mmoja amemfanya kujua jukumu lake katika timu. Hans, mlinda mlango wa zamani wa Holland ameifanya Yanga icheze mpira wa kuvutia sana huku wakiwa wagumu kufungika katika VPL. Hiki ndicho alichoiwezesha Yanga kufanya na ndiyo maana amefanikiwa mno katika mwaka wake mmoja na nusu klabuni hapo.
Hans si mtu wa kujijali mwenyewe bali yeye ana mtazamo wa timu na jinsi ya kuinua viwango vya wachezaji wake. Amekuwa na mtazamo sahihi katika sajili zake chache alizofanya klabuni hapo. Mlinzi wa kushoto kijana Mwinyi Hajji alimsaini wakati wa usajili wa majira ya kiangazi mwaka uliopita baada ya kumuona mchezaji huyo katika michuano ya Mapinduzi Cup akiwa na kikosi cha JKU ya Zanzibar mwezi Januari, 2015.
Kiungo, Thabani Kamusoko na mshambulizi, Donald Ngoma wote wamesajiliwa na Hans msimu huu baada ya kuwaona Wazimbabwe hao walipocheza dhidi ya Yanga katika michuano ya Shirikisho Afrika mwaka jana wakiwa na Platnum Stars.
Deus Kaseke ni chaguo lake lingine alilosajili Yanga baada ya kuvutiwa na kiungo huyo wa pembeni wa zamani wa timu ya Mbeya City FC, kijana Geofrey Mwashuiya yeye alisajiliwa haraka kutoka timu ya daraja la kwanza Kimondo FC ya Mbeya baada ya Hans kumuona kijana huyo Yanga ilipokuwa katika maandalizi ya msimu huko Mbeya mwezi Agosti, 2015.
Hao ni baadhi tu ya wachezaji waliotazamwa kwa ‘macho makali’ ya Hans na wote wanacheza vizuri huku wakitoa msaada mkubwa kwa timu hiyo.
Hans ni kama amejijengea hisia za ndani za kushindwa kukubali kushindwa katika timu ya Yanga. Ujuzi wa Hans katika mbinu umeng’ara msimu huu kwani timu yake inafunga magoli mengi na kuruhusu machache.
Hans ni kama amejijengea hisia za ndani za kushindwa kukubali kushindwa katika timu ya Yanga. Ujuzi wa Hans katika mbinu umeng’ara msimu huu kwani timu yake inafunga magoli mengi na kuruhusu machache.
Kitu kingine kinachompa mafanikio ni kujali muda. Hans ameboresha vilivyo ubora wa kikosi chake kwa kuwasajili wachezaji mahiri ambao sasa wanahitaji kufanya vizuri katika dakika 180 tu ili wafuzu kwa hatua ya makundi ya CAF. Bila shaka anastahili sifa kwa kazi yake kubwa na nzuri anayoendelea kuifanya.
Na Baraka Mbolembole

No comments:

Powered by Blogger.