Tuhuma zamwandama Rais Magufuli
TUHUMA zimeendelea
kuelekezwa kwa Rais
John Magufuli kutokana na hatua yake ya kukwepa jukumu la
kutatua mgogoro wa kisiasa visiwani Zanzibar, anaandika Faki Sosi.
Peter Lijualikali, Mbunge wa Jimbo la Kilombero (Chadema) amesema,
hatua yake ya kuupa mgongo mgogoro huo inaashiria kuitenga Zanzibar.
Akizungumza na
Mwanahalisi Online leo Jijini Dar es Salaam alipokuwa kwenye uzinduzi wa
programu ya kuwezesha umulikishaji Ardhi, amesema kuwa, hatua hiyo ni ‘utoto wa
kisiasa’ na kwamba, yeye kama Raia wa Jamhuri ya Muungano hawezi kuepuka
mgogoro huo.
Akiwa kwenye Mkutano
na Wazee wa CCM Mkoa wa Dar es Salaam wiki iliyopita, Rais Magufuli alisema
kwamba, hatoingilia mgogoro huo kwa madai unapaswa kutatuliwa na Tume ya
Uchaguzi ya Zanzibar (NEC).
Kauli yake imepingwa
na kada mbalimbali nchini zikidai kuwa, anachokifanya rais huyo ni kukimbia
majukumu yake sambamba na kutaka kukiokoa chama chake (CCM) kilichoshindwa
kwenye uchaguzi wa Zanzibar uliofanyika tarehe 25 Oktoba 2015.
Lijualikali amesema, kauli
hiyo inaashiria uvunjifu wa Muungano kutokana na kuyatenga masuala ambayo
angeweza kuwajibika kama amiri jeshi mkuu.
No comments: