Magufuli agonga mwamba Z’bar
LICHA ya kauli za vitisho zilizotolewa
na Rais John
Magufuli wakati akizungumza na wazee wa Chama Cha Mapinduzi (CCM)
jijini Dar es Salaam wiki iliyopita kwamba, atawashughulikia watakaoleta
fyokofyoko, Wazanzibari wamepuuza, anaandika Faki Sosi.
Kassim Bakar Ali, Mwenyekiti wa Jahazi Asilia ambaye pia alikuwa
mgombea urais Zanzibar kwenye uchaguzi wa tarehe 25 Oktoba mwaka jana amesema,
Zanzibar ina historia ya migogoro ya kisiasa.
Amesema, imekuwa
kwenye migogoro ya uchaguzi tangu mwaka 1957 na kwamba, jeshi halikuweza
kuiondoa hivyo kuamini nguvu ama kutumia jeshi ndio muafaka ni kuchemsha.
Kassim ameonya
kwamba, kutumia jeshi kutachangia kuchochea mgogoro wa kisiasa na hata
kusababisha machafuko visiwani humo.
Amesema yeye na
chama chake hawana imani na jeshi hilo kwa kuwa nao hushiriki katika kuiba kura
“hatunaimani na jeshi kutokana na kuwa wao ni wasisimamizi wa wizi wa kura.”
Faki Rashid
Maalim Mkazi wa Bububu, Unguja amesema, kilichofanywa na Rais Magufuli ni
kuwatia hofu Wazanzibari na wao wametambua hilo.
“Alitumia maneno
yale kutia hofu tu, lakini hakuna asiyejua kwamba CCM wanaitaka Zanzibar kwa
gharama yoyote lakini pia naamini kwamba, haki hutafutwa na Wazanzibari
wakiamini hilo hawatakuwa na hofu,” amesema na kuongeza;
“Tunajua ni
vitisho tua, hata alipoanza kwa kutaja sijui Dodoma, Nachingwea, Ukerewe lakini
mwisho wa kauli alifikia kwenye kiini chake na kuitaja Pemba na Zanzibar kwa
maana ya Unguja kuwa ndio kuna mateso ya kisiasa.”
Hata hivyo,
Abdallah Kombo Khamis, aliyekuwa mgombea wa urais kupitia Chama Democratic Part
(DP) amesema, kauli ya Rais Magufuli kwamba hausiki na suala la Zanzibar huku
yeye akiwa Amiri Jeshi Mkuu ni kukimbia majukumu.
“Yeye ni Amiri
Jeshi wa Tanzania au wa CCM? kwani amekuwa akikitumikia chama chake bila kujali
maslahi ya wananchi wake,” amehoji Kombo.
Amesema kuwa,
wananchi wa Zanzibar tayari wamezoea kuonewa na kupigwa kama walivyofanyiwa
miaka iliyopita.
“Mimi mwenyewe
ni muhanga wa machachuko na vurugu zilizowahi kutokea miaka iliyopita kwani
nilipoteza kaka yangu kwa kupigwa risasi na askari na mjomba wangu kupigwa
risasi ya mguu mpaka leo ni mlemavu,” amesema Kombo.
Seif Ali Iddi
aliyekuwa mgombea kupita chama NRA amesema kuwa, Wazanzibari wapo njiapanda
kutokana na Rais Magufuli kukwepa kutatua mgogoro wa kisiasa visiwani humo.
Amesema kuwa,
Rais Magufuli anakwepa kuhusika kutokana na kuwa chama kilichomuweka madarakani
ndicho kinachoshika sukani wa dhuruma visiwani humo huku akibainisha kuwa,
mgogoro wa kisiasa viswani humo ni wa kihistoria.
Chanzo Mwananchionline
No comments: