CCM yazidi kutengwa Z’bar
John Magufuli, Rais wa Tanzania, akiteta jambo na Dk. Ali Mohamed Shein, Mgombea Urais wa Zanzibar kwa tiketi ya CCM
ORODHA ya vyama vinavyopingana na Chama Cha Mapinduzi
(CCM) kurudia uchaguzi visiwani Zanzibar inazidi kuongezeka, anaandika Happyness Lidwino.
Chama cha ACT-Wazalendo kimeingia kwenye orodha ya vyama
vinavyopinga marudio hayo na kufanya idadi ya vyama vinavyogomea kuongezeka na
kuwa tisa kati ya 14 vilivyoshiriki katika uchaguzi huo wa tarehe 25 Oktoba
mwaka jana.
ZEC ilitangaza marudio ya uchaguzi
huo kuwa tarehe 20 Machi mwaka huu baada ya mwenyekiti wake, Jecha Salim Jecha
kufuta matokeo ya uchaguzi wa Oktoba mwaka jana kwa madai ya kugubikwa na
kasoro.
Hatua hiyo imepingwa na baadhi ya
wananchi, wanataaluma, wanasisa na taasisi ndani ya nchi pia mataifa ya nje
ikiwa ni pamoja na Umoja wa Ulaya (EU) pia Marekani.
Kwenye uchaguzi huo wa awali, Maalim
Seif Shariff Hamad, Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF), alitangaza matokeo
yake yaliyoonesha kuwa amemshinda mpinzani wake wa Chama Cha Mapinduzi (CCM),
Dk. Ali Mohamed Shein, Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi visiwani humo.
Kauli ya ACT-Wazalendo imetolewa na
Zitto Kabwe, Kiongozi Mkuu wa chama hicho baada ya kuwepo kwa makubaliano
yaliyofanyika kwenye Kikao cha Kamati Kuu ya chama hicho kilihitimishwa jana
Jijini Dar es Salaam.
Kamati hiyo imetoa msimamo wa
kutoshiriki uchaguzi huo na kutoa wito kwa Dk. John Magufuli, Rais wa Tanzania
kuchukua hatau stahiki kwa mamlaka aliyopewa kikatiba kuliko kukimbia jukumu
lake.
Akizungumza na waandika ofisini
kwake Zitto amesema, Kamati Kuu pia inataka madiwani na wawakilishi walioshinda
katika uchaguzi wa tarehe 25 Oktoba mwaka jana kutangazwa na ZEC ili
watambulike na kuanza kuwatumikia wananchi.
Zitto amesema, Kamati Kuu imeendelea
kusisitiza kuwa Jecha hakuwa na uhalali wa kisiasa, kikatiba na kisheria
kuufuta uchaguzi Zanzibar.
“Dalili zote za kisiasa zinaonesha
kuwa Jecha alichukua hatua ile kwa shinikizo au kwa mapenzi ya kisiasa kwa
lengo la kuzuia ushindi wa chama kimoja ambacho kilikua na dalili ya kushinda.
“Mbali na CCM, waangalizi wote wa
uchaguzi wa ndani na nje pamoja na jumuiya za kimataifa wametamka bayana kwa
uchaguzi wa Zanzibar ulifanyika kwa haki, huru na demokrasia na matokeo ya
uchaguzi huo yalizingatia utashi wa wapiga kura,” amesema Zitto.
“Kamati kuu pia tunaamini kwamba
suluhu ya mkwamo wa kisiasa Zanzibar ni kufanya mazungumzo yatakayojumuisha
wadau wote muhimu katika mchakato wa uchaguzi wa Zanzibar. Hatuamini kwamba
mkwamo huu utatatuliwa kwa vitisho vya dola,” amesema
No comments: